Jumatano 17 Desemba 2025 - 20:00
Kukuza Utamaduni wa Swala Hakufanyiki Kulingana na Amri

Hawza/ Ayatullah Nouri Hamadani, akisisitiza juu ya umuhimu wa kujenga utamaduni kuanzia katika mazingira ya elimu na familia, amesema wazi kuwa: kukuza utamaduni wa Swala hakutapatikana kwa amri. Ikiwa tutajenga utamaduni na faradhi hii ya Mwenyezi Mungu ikawasilishwa kwa sifa zilizoelezwa, bila shaka nuru yake itakuwa na athari.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, matini kamili ya ujumbe wa Ayatullah Nouri Hamedani katika Mkutano wa Kumi wa Swala, uliofanyika leo Jumatano tarehe 17 December 2025, katika Ukumbi wa Ayatullah Shar‘i (r.a), Makao Makuu ya Usimamizi wa Hawza za Wanawake, ni kama ifuatavyo:

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Salamu na heshima zielekee kwenye mkusanyiko huu mtukufu na wa kiroho.

Swala ni miongoni mwa wajibu muhimu zaidi, au tuseme wajibu mkuu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu alioutilia mkazo mkubwa. Jambo la kutafakari ni kwamba; pale Mwenyezi Mungu anapoamrisha kusimamisha Swala, pia katika aya nyingi za Qur’ani hutaja athari na faida zake.

Ni lazima kutambua kuwa mkazo huu ni kwa sababu gani na athari zake zitaonekana kwa namna gani. Bila shaka sifa hizi si kwa ajili ya usahihi wa Swala pekee; kwa sababu kila mtu anapaswa kusimamisha Swala kwa usahihi.

Swala inayokubaliwa ni ile ambayo athari zake huonekana katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii; yaani, mwenye kusimamisha Swala anapaswa kunufaika na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: “Hakika Swala humzuia mtu na mambo machafu na maovu”, na Swala iwe kwake ni mi‘raji (ngazi ya kupaa kiroho). Ikiwa hali itakuwa kinyume na hivyo, basi itakuwa mfano wa kauli: “Ole wao wanaoswali.”

Inapaswa kuzingatiwa kuwa; njia ya kufikia kila aina ya kheri na ya kujilinda na dhambi na maasia ni kusimamisha Swala kwa sifa tulizozitaja. Njia iliyo karibu zaidi ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu pia ni njia hii—ya Swala.

Mimi ninaamini kuwa Swala inayochanganywa na utekelezaji wa maelekezo ya Qur’ani Tukufu na mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s) humfanya mwenye kuswali kufikia daraja ya juu ya kiroho.

Leo, kuhimiza na kutia moyo kusimamisha faradhi hii ya Mwenyezi Mungu ni jambo jema na lenye athari, lakini ni lazima ujenzi wa utamaduni uanze katika mazingira ya elimu na familia, na uhusiano wa moyo na faradhi hii uimarishwe. Inapaswa kufahamika kuwa kukuza utamaduni wa Swala hakutapatikana kwa amri na lazima. Tukijenga utamaduni, na faradhi hii ya Mwenyezi Mungu ikawasilishwa kwa sifa tulizozitaja, bila shaka nuru yake itakuwa na athari chanya.

Insha’Allah, wapendwa wanaojituma katika jukumu hili tukufu—hasa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Qira’ati, ambaye ametumia maisha yake katika kueneza maelekezo haya ya Mwenyezi Mungu—wapate mafanikio. Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie wote taufiki.

Hussein Nouri Hamedani

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha